CHANGAMOTO ZA MAFUNUO KATIKA ENEO LA KUOA NA KUOLEWA KWA VIJANA WA KIKRISTO
Bwana yesu asifiwe mpendwa, nakusalimu katika jina la Yesu aliye Bwana na mwokozi wa maisha yetu.
Karibu katika makala yetu hii ya AMKA UKUE KIROHO ambapo leo tutakwenda kuangalia changamoto ya mafunuo katika eneo la kuoa na kuolewa kwa vijana wa kikristo. Namshukuru Mungu kwa ajili yako maana ni kwa neema tu hata upate nafasi hii ya kusoma somo hili ambalo lina leta utukufu kwa Mungu kwa vijana wake wanao mtii. Hivyo andaa moyo wako kwa ajili ya kupokea kile ambacho Roho Mtakatifu atakusemesha ndani yako katika kukuvusha katika maeneo mbalimbali ya ujana wako. Karibu tuanze sote katika somo hili ;-
Utangulizi; Ili uweze kujifunza vizuri kupitia somo hili ni LAZIMA uondoe hali ya kujihukumu ndani yako kama umewahi kufanya Kosa katika hili eneo.
Swala la mafunuo ni changamoto kubwa sana kwa kanisa hasa linapofika swala la vijana waliookoka kutaka kuoa na kuolewa. Changamoto kubwa inatokana na aina mbili za uwasilishaji hoja kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine(mwanaume na mwanamke),yaani vijana wengi husema kuwa;
- Mungu amesema(amenionyesha) kuwa wewe ni mume wangu au mke wangu. Moyoni mwangu najisikia amani ya kuishi na wewe (Mimi binafsi natamani kuishi na wewe)
- Aina hizi mbili za kuwasilisha hoja kati ya mwanaume na mwanamke ndio zimeleta vilio na majeraha kwa vijana wengi wa Kikristo. Wapo walioumizwa sana na kufikia hatua ya kuwachukia wanawake wote au wanaume wote na kutowaamini kabisa kutokana na makosa yaliyofanywa na baadhi ya vijana kwa wenzao.
Vijana Wengine hawataki tena kusikia habari ya kuolewa au kuoa tena.Vijana wengine hawataki kabisa kusikia habari za watu waliookoka na habari za mafunuo. Hii inatokana na kuumizwa kwa sababu ya mafunuo
- Mtu anaposema kwa mtu mwingine kuwa Mungu amesema au amenionyeshakuwa wewe ni Mke/mme wangu, neno hili ni zito sana linahitaji uhakika mkubwa sana wa Ki Mungu ili kuona kama lina ukweli ndani nyake. Neno hili Lina nafasi kubwa ya kubadili fikra za mtu aliyeambiwa ujumbe huo na Mara nyingi mtu aliyeambiwa anajikuta kwenye wakati mgumu sana hasa akijilinganisha kiwango chake cha kiroho na kiwango cha mtu aliyemwambia hilo neno.
- Neno hili lina nafasi kubwa sana ya kupunguza mzigo wa kumuuliza Mungu kwa maombi juu ya mtu aliye pewa ujumbe yeye binafsi juu ya usahihi wa hilo jambo kwa mtu aliyeambiwa, hasa inapoonekana Mungu anachelewa kujibu. Neno hili limekuwa ni changamoto kubwa sana kwa kanisa. Inawezekana mtu aliyeambiwa neno hili alikuwa katika kipindi cha kuomba Mungu amsaidie ili apate mume/mke, sasa akitokea mtu wa kumwambia kuwa Mungu amenionyesha au ameniambia kuwa wewe ni mume wangu au mke wangu basi ni rahisi akafikiri kuwa Mungu ameshamjibu tayari maombi yake, ingawa wakati mwingine shetani hutumia mlango huu kuwapoteza wengi. Sio kwamba Mungu huwa hasemi na watu wake, *ILA* shida kubwa ni namna ya kumuelewa Mungu anaposema na hao watu wake. Swala la Kusikia na kuelewa sauti ya BWANA ni shida kubwa sana kwa watu waliookoka. Ndio maana kuna wakati ambao unakuta mtu mmoja anasema jambo kuwa Mungu aniambia hivi na mwingine anapingana nae huku akisema kuwa nae ameambiwa na Mungu.
Napenda niseme hivi pia, kutafsiri maono ambayo yanakuja ni changamoto kubwa pia kwa watu wa Mungu. Wengine wanatafsiri harakaharaka kwa kutumia akili zao na mwisho wa siku husababisha vilio kwenye maisha ya watu wengine.
Sio aina zote za mafunuo yanayokuja kwako huwa yanatoka kwa Mungu Alie Hai katika Kristo Yesu. Mafunuo mengine yanatoka kwa shetani mwenyewe.
2Wakorintho 11:14 "Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru"
_*✳Kumbuka:* Unapotaka kuoa au kuolewa ndani ya mapenzi ya Mungu ili umzalie matunda kupitia wokovu wako aliokupa basi vita yako inakuwa ni kubwa sana na shetani anapambana sana na wewe kwa kupitisha mafunuo yake kwako ili aweze kukuvuruge.
Kila ufunuo unaokuja kwako ni *LAZIMA* uupime kwenye neno la Mungu. Shida nyingine ni kwamba watu wengi ni wavivu kusoma neno la Mungu na wengine wanasoma kama magazeti na hivyo wanashindwa kupambanuo mafunuo ya roho. Wakati mwingine mwanaume au mwanamke anajikuta amefuatwa na watu wawili au watatu au wanne na wanakuja kwa lengo la kuoana, na kila mmoja anasema Mungu amemuonyesha au amemsemesha kuwa huyo ni mume wake au mke wake kitu ambacho unaona wazi kabisa kuwa shetani yupo kazini. Mungu gani huyo anaye jifunua kwa watu wengi kwa lengo moja la ndoa kwa mtu mmoja??
✳USHUHUDA:* Kuna kipindi fulani hivi niliwahi kuombwa ushauri na wasichana watatu ambao walikuwa wameokoka na wameumizwa kwenye mahusiano na kijana mmoja hivi ambae alikuwa akihubiri maeneo mbali mbali, na kila msichana kati ya hawa alinitafuta kwa wakati wake na kila mtu hakujua kama mwenzake nae ameumizwa. Nilichokuja kushangaa ni kwamba kila msichana nikimuuliza kuwa huyo mwanaume aliyekuumiza na kukuacha anaitwa nani akawa anataja jina lile lile la yule kijana. Na yule kijana alikuwa anatumia vibaya huduma aliyokuwa amepewa na Mungu ya kuhubiri kwa ajili ya kuwadanganya wasichana kuwa Mungu amemsemesha. Hii ni hatari sana.
_✳KUMBUKA:*Mungu aliye hai huwa hajichanganyi na mafunuo yake na neno lake, ila watu wake ndio wanajichanganya wenyewe na wanaanza kumsingizia Mungu kuwa amebadilisha mpango.
- Moyoni mwangu najisikia amani ya kuishi na wewe(mimi binafsi natamani kuishi na wewe)*. Kijana!, Kama hauna uhakika kuwa unachotaka kufanya kimetoka kwa Mungu au kimetoka kwako binafsi, ni VYEMA ukamwambia mtu ukweli kuliko ukamsingizia Mungu.Gharama yake ni kubwa.
Baada ya muda kupita, matokeo yatathibitisha kama kweli ni Mungu Alie Hai ndie aliyekuwa amesema na wewe au ni wewe mwenyewe au shetani ndio alijifunua kwako. Kumbuka
Kuna wakati ambao;_
I). Nafsi yako inaongea na sio Mungu aliyeongea ndani yako.
II) Moyo wako unatamani na sio Mungu aliyekusemesha. Yeremia 17:9 *Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?"
III). Akili yako ndio inayoamua na sio Mungu aliyekutuma
IV). Macho yako yamemtamani mtu na sio Mungu aliyeongea nawe.
Hayo mazingira yanaweza yakatokea kwa mtu na akafikiri kuwa ni Mungu aliyeongea nae.
ZINGATIA MAMBO YAFUATAYO ILI YAKUSAIDIE.
- USIANGALIE TU VIWANGO VYA KIROHO ALIVYONAVYO MTU AU HUDUMA ALIYONAYO MTU ANAYEKUPA MAFUNUO.
Hili jambo linawagharimu zaidi wasichana wengi. Baada ya kupewa ufunuo na vijana wanajikuta wanakosa ujasiri wa kuwakatalia ili wapate muda wa kumuomba Mungu wao binafsi ili awathibitishie usahihi wa hilo jambo. Unaweza ukamuona mtu yuko vizuri sana kiroho lakini akifika wakati wa kuoa anatumia akili zake hasa akiona Mungu anaonekana amechelewa kumjibu.
Pia wako vijana wengi sana ambao wanatumia neema ya vipawa walivyopewa na Mungu kwa ajili ya kuwadanganyia wasichana na kuwapata kirahisi.* Na mwisho wa siku unakuta kijana amewajaza vilio wasichana wengi baada ya kuwachezea na kuwaacha.
_*✳USHAURI*: Ukipewa ufunuo na mtu juu ya jambo la kuoa na kuolewa na bado Mungu hajathibitisha kwako, mimi mtumishi wa Mungu nakushauri usimkubalie kabisa, nasema tena usikubali, hata kama anaonekana yuko vizuri sana kiroho. Gharama yake ni kubwa sana.
_*☑ZINGATIA:*Kama kweli Mungu amesema nae na jambo hilo limetoka kwake Mungu mwenyewe basi atalithibitisha na kwako pia. Yohana 8:17 "Tena katika torati yenu imeandikwa kwamba, Ushuhuda wa watu wawili ni kweli." Kwanini Mungu aseme na yeye peke yake na asikusemeshe na wewe wakati hayo maamuzi yanahusu future yako na hatma nzima ya kesho yako ????*No no no no ‼
Usifanye makosa ya kumkubalia mtu kama hauna uhakika na baada ya kuingia nae mahusiano ndipo ukaanza kumuuliza Mungu, kwasababu nguvu ya upendo ikiingia kwa watu;
I). Inafunga masikio na kuwafanya wasisikie_
II).Inapofusha macho na kuwafanya wasione_
Wimbo Ulio Bora 8:6".....kwa maana Upendo una nguvu kama mauti.." Hivyo hata Mungu akisema inakuwa ni vigumu sana kumsikia na kumuelewa,ndio maana mara nyingi sana Mungu huwa anakaa kimya watu wakianza kumuuliza huku wameshafanya maamuzi tayari.
2. CHUNGUZA VIZURI AMANI INAYOAMUA MOYONI MWAKO UNAPOKUWA UNAINGIA MAKUBALIANO YA KUONA NA MTU.
Kabla ya kufanya maamuzi ya kuingia mahusiano na mtu, chunguza vizuri aina ya amani inayoamua ndani yako. Neno la Mungu linasema kuwa "Amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu".(Wakolosai 3:15).
Sio kila aina ya amani inayoamua ndani ya mtu basi ni amani ya Kristo. Ulimwengu pia huwa unatoa amani(Yohana 14:27). Ni vigumu sana kwa mtu kutambua amani ya Kristo kama hasomi neno la Kristo/Mungu.
Wakati mwingine kwenye huduma nimekutana na vijana ambao wamefika mahali pagumu sana kwenye mahusiano yao. Kijana anasema mtumishi sina amani kabisa moyoni mwangu na haya mahusiano, na nikimuuliza kwamba mwanzoni wakati unakubaliana na huyo mtu ilikuwaje? anasema nilikuwa na amani sana sana mtumishi lakini nashangaa kwasasa sina amani kabisa. Huwa nagundua kuwa hakutulia vizuri wakati anafanya maamuzi na Kuna uwezekano sio amani ya Kristo iliyokuwa imeamua ndani yake.Wakati mwingine ni tamaa tu.
KUUGUA KWA ROHO MTAKATIFU*_
Kuugua ni mzigo ambao unabebwa moyoni mwako, ambao ni mchanganyiko wa kukosa amani na kukosa furaha. Mara nyingi Roho Mtakatifu anaugua ndani yako iwapo Kuna maamuzi ambayo unataka kufanya na hayako sawasawana kusudi la Mungu. Unapoona unataka kumkubalia mtu ili uingie kwenye mahusiano halafu unasikia kukosa amani/Roho Mtakatifu anaugua ndani yako ni ISHARA kwamba kuna kitu hakiko sawa juu ya maamuzi yako, na hivyo pata muda wa kuendelea kumuuliza BWANA.
Mara nyingi sana Mungu anasema na vijana kwa njia hii lakini wanashindwa kuelewa na wanaishia kusema Mungu hakuwahi kuwasemesha na wanamlalamikia baada ya mambo kuharibika huko mbeleni.
Unakuta mwanaume au mwanamke anakosa amani kabisa na anasikia Roho Mtakatifu anaugua ndani yake lakini anaendelea kujilazimisha tu. 2Wakorintho 3:17 "..... alipo Roho wa BWANA hapo ndipo penye uhuru".
Hiyo huzuni haiwezi kuisha ndani yako hadi urudi kwenye kusudi la Mungu na ukiendelea kukaa kwenye mahusiano ambayo yako nje ya kusudi la Mungu utajikuta unapata amani kidogo lakini huzuni inakuja tena.
Mtu Mwingine anajikuta kila akikutana uso kwa uso na huyo mwanaume/mwanamke huzuni ndio inazidi au kila akiongea nae kwenye simu anasikia huzuni moyoni mwake. Muulize vizuri Mungu juu ya maamuzi yako unapoona hali za namna hii._
3. ANZA UPYA KAMA UMEFANYA MAKOSA NA BADO HAUJAINGIA KWENYE AGANO LA NDOA.
Wakati mwingine unakuta kijana anaogopa kurudi upya kwa Mungu baada ya kuona amekosea kufanya maamuzi hasa kwa kuogopa wapendwa kwamba watamwelewaje. Inawezekana mwanzoni aliwaambia kuwa Mungu amenionyesha/amenifunulia mtu fulani ni mke wangu au mume wangu hivyo anaogopa namna ya kuwaambia tena kuwa alikosea na pengine hakumuelewa vizuri Mungu.
Ndio maana nawaambia vijana kuwa, kama hauna uhakika kuwa ni Mungu aliyeongea na wewe punguza mbwembwe kwa wapendwa kwasababu kama utakosea utajiweka mahali pagumu sana.
Ni bora uingie gharama ya kuvunja hayo mahusiano lakini uingie kwenye kusudi la Mungu. Ni kweli kabisa binadamu hawatakuelewa kirahisi na wanaweza wakakucheka lakini Mungu atakuelewa kuwa mtoto wake ulikosea na unahitaji msaada mkubwa kutoka kwake.
Utapata shida mwanzoni na pengine kudharauliwa na kuchekwa na marafiki zako/wapendwa, lakini bora ufanye hivyo ili ujenge kesho yenye furaha zaidi.
Fanya hivi;
I).Tubu kwa Mungu ili akusamehe.
II). Muombe msamaha mtu unayeachana nae.
III).Vunja agano la maneno na futa viapo ulivyokuwa umeingia na huyo mtu.
*✳KUMBUKA:* Mahusiano sio agano kamili na hivyo yanaweza kuvunjika. *Jambo la muhimu ni kwamba unatakiwa utafute hekima ya Mungu namna ya kuvunja hayo mahusiano ili kuzuia mambo ya kumwachia maumivu mengi mtu uliyekuwa nae na kuondoa hali za chuki na uadui.*
Baada ya kufanya maamuzi kama hayo,Pata muda mzuri wa kumuomba Mungu zaidi kwa ajili ya jambo hili ili usikosee tena na usije ukafanya maamuzi kwa kukosea tena.
*✳ZINGATIA:* MUNGU akikupa neema ya kujua kuwa uko kwenye mahusiano ambayo yako nje ya kusudi lake kabla ya kufanya agano la ndoa halafu ukaamua kuendelea tu na hiyo safari, nakuambia kuwa utaingia gharama za ajabu sana huko mbeleni,hivyo ni bora urudi upya kwa Bwana Yesu.
Uwe mwangalifu sana katika mafunuo ya ndoa
Somo hili limefundishwa Na mtumishi wa Mungu_
Mwl M. Mwambeso,* chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu
Mpendwa njia rahisi ya Mungu kushugulika na mahitaji yako ni kumtegea yeye katika ujana wako ni kuokoka, kama bado hauja mwamini Yesu au ulikuwa umeokoka na ukarudi nyuma Sali paoja nami sala hii ya toba na Mungu atakusamehe na kuku safisha Dhambi zako zote. Hakikisha unapo omba toba hii omba kwa kumaanisha na umalizapo usirudie dhambi tena bali mfuate Mungu ili ajidhihirishe katika maisha yako kwa uweza wake wote.
Comments
Post a Comment