ASILI YA MWANADAMU KIBIBLIA (Biblical anthropology) 3


Bwana yesu asifiwe, nakusalimu katika jina la Yesu aliye Bwana na mwokozi wa maisha yetu.
 Karibu katika makala yetu hii ya AMKA UKUE KIROHO ambapo leo Tutaendelea na somo Linaloitwa "ASILI YA MWANADUMU KIBLIA", katika sehemu ya kwanza tulijifunza mambo mengi sana, na si rahisi kuyarudia, hivyo kama haukujifunza nakuomba ulipitie na kulisoma kwa ajili ya Utukufu wa Bwana.

Somo letu kumbuka linamwangalia mwanadamu alivyo kibiblia kuanzia kuumbwa kwake, sababu za kuumbwa kwake, asili yake, uwezo uliyo ndani yake, hatma yake na kadhalika.

Ni mambo ya muhimu na ya msingi sana kuyajua kama kweli wewe unataka kuwa mwanafunzi wa kweli wa Yesu kwa sababu Yesu hakuwahi kuishi kiolela alipokuwa hapa duniani bali kila wakati alihakikisha yupo ndani ya kusudi la yeye kuwepo.

Sehemu ya kwanza kabisa tuliona maswali ya muhimu sana katika kujijua ili maisha yako kwa namna yeyote uyaongezee thamani kwa kuliishi kusudi lako.

Tuliangalia haya maswali matano;
Nimetoka wapi?

1.    Mimi ni nani?
2.    Kwanini niliumbwa?
3.    Ninaweza nikafanya nini?
4.    Hatma yangu ni nini?

Ninaamini mpaka sasa unao uelewa mpana sana wa haya maswali, na kama umenifuatilia nimeyajibu mengi hapa tayari kwenye muendelezo wa hili somo.

 Leo nataka tuangalie kidogo kwenye hili somo kuhusu Kusudi la Mungu ngazi ya pili kama nilivyokuambia nimeligawanya hivyo, kwamba ile sababu binafsi ya wewe kuumbwa ni ipi?

KUSUDI ndilo maisha ya mtu na maisha ya mtu ndilo kusudi la yeye kuumbwa.

Huwa nasema hivi “Mungu huwa anaumba kusudi, halafu kusudi linamuumba mtu” Kwa maneno mengine, kilichosababisha Mungu akuumbe ni baada ya kuona uhitaji wa kitu fulani kukamilika au kufanyika hapa duniani, ndipo akaitengeneza inaitwa kusudi; akaanza kuangalia mtu wa kulibeba hilo kusudi ndipo akakupata wewe.

Kwa hiyo ukiweza kujijua kusudi la maisha yako, basi umeyapata maisha yako
KUSUDI NI NINI?
Ni sababu ya wewe kuumbwa na kuzaliwa hapa duniani.

Ni ile sababu ya wewe kuwepo kwenye kizazi hiki, kuzaliwa Tanzania au nchi uliyozaliwa, kuzaliwa kwenye hiyo familia, kuzaliwa na hiyo sura yako, kuzaliwa na hilo umbo lako….nk

Kusudi linatengeneza wito…..
Mungu alikuleta kutoka alikokuwa amekuweka ili uje kutimiza kazi fulani.

WITO - ni haja iliyopo inayomsukuma anayeitaka ifanikiwe akiite.
Kusudi ni sababu ya wewe kuumbwa lakini inaanza kuhesabiwa pale unapozaliwa hapa duniani.
Kuzaliwa ni wito kabisa, ile kwamba umezaliwa maana yake umeitwa tayari na Mungu kwa sababu ameona uhitaji wa kitu ambacho ameshakiweka ndani yako ili ukakifanye hapa duniani.

Hebu fikiri ni wangapi leo hii wanajua kwanini walizaliwa na wanafanya nini kulingana na vile walivyoitiwa kuvifanya?

KUSUDI linalenga wajibu wako ambao Mungu anataka aukamilishe hapa duniani, kwa hiyo anamtafuta mtu wa kulikamilisha ndiyo lazima aweke ndani yako wa kukamilisha kile alichokutuma kukifanya hapa duniani.

Unapoishi kwa kufanya kile ulichojaliwa uwezo nacho kukifanya na kukifanya katika njia sahihi hapo ndo tunasema unaliishi kusudi.
Watu wanaposhindwa kujua kusudi la maisha yao au vitu walivyonavyo na vilivyowazunguka, ndipo  inatokea uharibifu kila siku.
Kama hujui kwa nini uliumbwa mweusi utaanza kujichubua ili uwe mweupe, kama hujui kwa nini ulipewa ilo umbo nzuri utaanza kuwa malaya maana utasumbuliwa na wanaume sana.
Kama hujui kwanini umepewa huo uwezo wa kuimba utautumia kuinua na kutangaza kazi za kidunia na uovu na hatimaye kusababisha maadili yaporomoke sana kwa jamii yako.

Fikiri ni watu wangapi leo hii Mungu aliwapa vipaji mbalimbali ikiwepo nguvu ya ushawishi ndani yao na wameitumia kuharibu jamii kubwa ya wanadamu, kwa kile kile Mungu alichowapa ili waijenge jamii badala yake imekuwa kinyume.
 KISUDI LINAKWENDA NA VITU VIFUATAVYO….*

1.    Mahali sahihi
2.    Kitu sahihi
3.    Muda sahihi
4.    Njia sahihi
Vinginevyo lile lile kusudi linaweza kugeuka likawa sumu kwenye maisha yako na ya wale waliyokuzunguka

Hiyo ni nguvu ya ajabu sana ya kiungu aliyoiweka kwa kila mwanadamu chini ya jua hata kama anajua au haujui, anamwamini Mungu au amwamini Mungu…….kanuni inafanya kazi kwa wote………..

 Kama unataka kujua kusudi la kitu chochote lazima umuulize aliye kitengeneza
Kwa mfano, huwezi kwenda kuulizia spea ya lap top yako ya dell wakati unatumiaToshiba…..kwa sababu ni kampuni mbili tofauti na zina miundo tofauti ya bidhaa zao.
Vivyo hivyo wewe unatoka kwa Mungu na chanzo chako ni Mungu, ukitaka kujua kwanini upo duniani muulize Mungu ndiye anayo majibu sahihi kwa ajili ya maisha yako

Hebu angalia hapa Mungu anavyosema,
 “Bwana, Mtakatifu wa Israeli, na Muumba wake, asema hivi; Niulize habari za mambo yatakayokuja; mambo ya wana wangu, na habari ya kazi ya mikono yangu; haya! Niagizeni. Mimi nimeiumba dunia, nimemhuluku mwanadamu juu yake; Mimi, naam, mikono yangu mimi, imezitanda mbingu, na jeshi lake lote nimeliamuru” ISAYA 45:11-12.
Yeye pekee ndiye aliyekuumba na yeye pekee ndiye mwenye taarifa sahihi zaidi kuhusu maisha yako, siyo wazazi wako wala mchungaji wako, wala mwalimu wako, au daktari au rafiki yako.
Hawa wanakusaidia tu kukupa taarifa sahihi kuhusu namna ya kumtafuta Mungu ili akupe majibu sahihi kuhusu maisha yako.

KUSUDI LINA UHUSIANO MKUBWA NA MUDA.

Kusudi limefungwa kwenye muda, ukicheza na muda wako unacheza na kusudi, na ukicheza na kusudi unacheza na maisha.
Kuna mambo mengine huwezi kuyafanya baada ya kuwa kijana, ulikuwa unayafanya utotoni tu. Pia ukisha kuwa mzee kuna mambo huwezi kuyafanya kama ulivyokuwa kijana.
Vivyo hivyo kusudi limefungwa  kwenye muda, lazima ujue muda wako una thamani sana na mtu yeyote aliyekwisha kujua kusudi la maisha yake anautunza muda sana na anauheshimu kweli kweli.

 Hebu angalia huu mstari;
Mhubiri 3:1 “Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu”
Kwa maneno mengine kila kusudi limefungwa ndani ya muda wake, huo muda ukiisha kusudi halifanyi tena kazi.

Yesu pia akasema;
Yohana 9:4 “Imetupasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenipeleka maadamu ni mchana, usiku waja asipoweza mtu kufanya kazi. Muda nilipo ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu”
Mchana wako ni kipindi cha uhai wako, ukicheza na muda huu uliyonao kusudi lako linabaki vile vile sijui utaenda kumjibu nini Mungu.

Anaposema muda aishipo hapa ulimwenguni yeye ni nuru ya watu, maana yake na wewe kumbuka Yesu alituita nuru ya ulimwengu na namna pekee ya kuwa nuru ya ulimwengu ni kule kuliishi kusudi la maisha yetu.

Sasa unaweza kuelewa ni wangapi wanaoishi wakiwa awaangazi kabisa na ndiyo maana dunia bado ipo gizani kwa sababu waliyoitwa kuwa nuru wameyakimbia majukumu yao ambayo ni kusudi la wao kuumbwa.
Kuna mengi sana hapa kuyaeleza lakini sina lengo la kuzama humu bali nakupa tu ufahamu mdogo ukusaidie. Nataka niongelee maono kidogo pia.

MAONO NI NINI?
Kwa sababu umeshaelewa angalau kidogo kuhusu kusudi ni rahisi kuelewa maono.

  • Maono ni kusudi la Mungu ndani ya moyo wa mtu anapoanza kuliona dhahiri ndani yake.
  • MAONO ni kuona kwa macho ya ndani mahali unapotakiwa ufike kulingana na kusudi lako.
  • Maono ni kufika hatua ya kujiona kama vile Mungu anavyokuona.
  • Maono ni kusudi katika picha ya ndani.

Kujua Kusudi lenyewe halitoshi unahitaji kuliona kwa upana wake kwenye moyo wako ili;-
Kukupa nguvu na shauku ya kulifikia
Kukupa nidhamu ya muda, Kukupa kujua watu sahihi na wasio sahihi kuambatana nao,  Kukupa kujua nini cha kukifanya na cha kutofanya ili kusudi lisife ndani yako.

NB; Mtu mwenye maono ana nidhamu ya hali ya juu na maisha yake kwa ujmla.
Mithali 29:18 “Pasipo maono, watu huacha kujizuia; Bali ana heri mtu yule aishikaye sheria”
Maono ni kitu cha msingi kwa maisha ya mtu kiasi kwamba kama huna maono hakuna atakayeweza kuona umuhimu wa maisha yako na maisha hayana maana bila maono.

Leo hii utakuta watu wengi wakiwa wanaishi maisha bila maono, rafiki yangu utaishi maisha ya utumwa maana kama wewe hauna maono itabidi kila wakati uishi kwa kutumikia maono ya wengine.
Tena kwako kila kitu kitakuwa sahihi na kila mtu kwako atakuwa sahihi.

Maono yana nguvu sana kiasi kwamba, yanakuchagulia maisha ya kuishi;.....
Maono yanakuchagulia mtu wa kuwa naye au kutokuwa naye-huwezi kuwa una maono halafu kila mtu akawa rafiki yako wa karibu, lazima uwe na marafiki wanaoendana na maono uliyo nayo.
Hata ikifika wakati wa kumchagua mwenzi wa maisha lazima maono yako yatumike kufanya hivyo na sii macho ya kawaida…….
Maono yanachagua nini cha kusoma, kusikia, kuona….huwezi kuwa na maono halafu unasoma magazeti ya udaku kila siku…...hapana vinginevyo utakuwa unayaua maono yako.

Maono yanakuchagulia nini cha kula na kunywa-ukishakuwa na maono tu lazima unakuwa makini kuutuza mwili wako maana unajigundua thamani uliyonayo na kwamba unahitaji kuwa na afya nzuri ili uyaishi maono yako, hutakunywa pombe kwa sababu ni dhambi tu, lakini hutakunywa pia kwa sababu ya uthamani wa mwili wako kujitunza kwa ajili ya maono uliyonayo.

Maono yanakuchagulia maneno ya kuongea, mawazo ya kila siku na nini cha kufanya……..maneno mengine unayoyaongea yanaua uwezo wa kuona aliyoweka Mungu moyoni mwako na hatimaye kuishi kama wanavyotaka dunia.

Kwa ujumla ,maono yanakuchagulia aina ya maisha ya kuyaishi na ni lazima uwe na nidhamu sana kuyafuata ndipo utafanikiwa.Kuna mengi sana hapa lakini kwakweli siyo lengo la hili somo kuzama sana huku, kwa wakati huu hiki kipande kidogo kinakutosha na pia itatusaidia kule tunakoelekea kwa ajili ya masomo mengine pia.

Furaha nzuri sana maishani ni kuishi maisha matakatifu yenye kumpendeza Mungu, na njia rahisi ya kuweza kuishi maisha matakatifu ni kumpatia Yesu maisha yako, yaani kuokoka. Unapo okoka Yesu anakuwa anayatazama maisha yako kwa ushindi ulio mkuu, huku akikutakasa kwa ajili ya uzima wa milele.

Kama bado hauja okoka sali sala hii fupi kwa imani, na utakuwa umekoka na kumpokea Roho Mtakatifu huku ukitembea kwa kuishi maisha matakatifu;-

Sema "Eeh Bwana Yesu, ninakuja mbele yeko, mimi ni mwenye dhambi, nimekutenda dhambi kupitia matendo yangu,  kusema kwangu, kuwaza kwangu na kwa dhambi za kujua na za kutokujua, Eeh Bwana Yesu ninaomba unisamehe, nisafishe kwa Damu yako ya thamani, nifute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uniandike jina langu kwenye kitabua cha Uzima wa milele, Eeh Bwana Yesu nakuja mbele zako kuanzia siku ya leo nifinyange moyo wangu, nafsi yangu na roho yangu kama upendavyo wewe, maisha yangu yote nakukabidhi wewe uyaongoze kwa Roho wako Mtakatifu, naomba na kuamini kupitia Jina la Yesu kristo aliye Bwana na mwokozi wa maisha yangu. Amina. 

Mpendwa kama umesali sala hii fupi kwa kumaanisha tayari umeupokea wokovu, unatakiwa utafute kanisa lililo karibu yako lenye kumuabudu Mungu wa kweli na uungane nao kwa ajili ya kukua kiroho. 

Kama umeguswa chochote kupitia makala hii , naomba uandika ujumbe wako hapo chini na nitakapo soma nitafurahia sana.

Na kama utahitaji maombi na ushauri wowote wa kiroho, wasiliana nami kupitia namba na emeil yangu kwa njia ya sms. mwishoni nitatoa namba na email,  lakini kama umeokoka kupitia makala hii waweza kunitumia ujumbe kwa njia ya simu , kwa watsapp, au kwa kawaida , au kupitia email yangu nitakayo itoa hapo chini.

Somo hili limeandaliwa na  Noel Pallangyo,  na kuandikwa na mwandishi Daniel J Mbugu wa makala ya AMKA UKUE KIRIHO.
Karibu katika sehemu ya Tatu ambayo itawekwa kupitia blogu hii. Mungu akubariki sana.
                     Wako mpendwa katika Kristo, 
                           Daniel Mbugu.
Kwa mwendelezo wa mafundisho zaidi ya neno la Mungu tembelea  AMKA UKUE KIRIHO. www.amkaukuekiroho1.blogspot. Na kwa ushauri kuhusiana na maisha ya wokovu tuma ujumbe katika email yangu. www.mbugudaniel@gmail.com. Au wasiliana nami kwa kutuma ujumbe kwa njia ya sms au whatsApp kwa 0758505174/ 0655505173.

Comments

Popular Posts