UTATU MTAKATIFU WA MUNGU (Holy Trinity) 1
Bwana yesu asifiwe, nakusalimu katika jina la Yesu aliye Bwana na mwokozi wa maisha yetu.
Karibu katika makala yetu hii ya AMKA
UKUE KIROHO ambapo leo tuta jifunza somo linaloitwa, UTATU
MTAKATIFU.
UTATU MTAKATIFU |
Wakati huu sasa, Bwana
ametupa neema nyingine ya kujifunza somo ambalo linamhusu Mungu wetu mmoja na
wa pekee tena wa kweli, ambaye anazo nafsi tatu lakini yeye ni Mungu mmoja tu
na wala siyo watatu.
Kati ya sifa nyingi na
za kipee aliyo nazo Mungu wetu ni UTATU MTAKATIFU. Hakuna miungu wengine mahali
kokote wa dini yeyote mwenye hii sifa. Utatu mtakatifu wa Mungu ni siri kuu
sana iliyositirika inayoelezea utendaji kazi wa Mungu kwa undani sana.
Kimsingi sisi kama wanadamu hatuna uwezo wa kuelezea utendaji wa Mungu ulivyo wala hata kumwelezea zaidi na vile tu alivyoamua kutufunilia kumhusu yeye.
Biblia iko wazi kabisa
kwamba sisi kama wanadamu tunafahamu kwa sehemu tu mambo ya Mungu na unabii.
Wakoritho 13:9 Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na
tunafanya unabii kwa sehemu;
Haya mambo ya Mungu tunayafahamu kwa sehemu tu maana Roho mtakatifu pekee ndiye anayeamua kutufunulia mambo ya Mungu kwa namna anavyotaka yeye.
Haya mambo ya Mungu
hakuna namna nyingine ya kuyafahamu kama siyo tu KUFUNULIWA na Roho wake; kwa
maneno mengine hatufahamu mambo ya Mungu kwa kusoma theolojia, au kusoma sana
biblia, au kuomba sana.
Tunayafahamu haya mambo
pale tu Roho mtakatifu anapoamua kutufunulia.
1Wakoritho 2:9 “lakini, kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo
jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa
mwanadamu,) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao. Lakini Mungu
ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu.
Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu
iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa
Mungu”
Nataka angalau kwa ufupi
tuangalie hii siri ya ajabu kuhusu utatu mtakatifu wa Mungu wetu wa pekee mmoja
na wa kweli.
NAFSI YA BABA, NAFSI YA MWANA, NAFSI YA ROHO MTAKATIFU;
Kwanza kabisa maandiko
yametuhakikishia sehemu nyingi tu kuhusu Utatu mtakatifu wa Mungu. Hebu
tuangalie baadhi ya maandiko kuhusu utatu mtakatifu;
1Yohana 5:8 “Kwa maana wako watatu washuhudiao mbinguni, Baba, na Neno, na Roho Mtakatifu, na watatu hawa ni umoja”
Mathayo 28:19 “Basi,
enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba,
na Mwana, na Roho Mtakatifu;”
Mathayo 3:16-17 “Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara
akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu
akishuka kama hua, akija juu yake; na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema,
Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye”
Hiyo ni baadhi ya mistari ambayo inaonesha kwa pamoja kuhusu uwepo wa nafsi tatu za Mungu, ukiangalia huo mstari wa mwisho hapo unaona hizi nafsi tatu kwa undani zaidi ten azote tatu zikiwa kwenye utendaji tofauti tofauti.
Ilisikika sauti kutoka mbinguni maana yake Mungu Baba, Yesu akiwa majini akiwa amebatizwa (maana yake nafsi ya pili Mungu mwana) na Roho wa Mungu akishuka kama huo (Maana yake nafsi ya tatu ya Mungu Mungu Roho mtakatifu)
Nitaifafanua zaidi
mistari hiyo yote kadei somo linavyoendelea,
Iko hivi; nafsi ya Baba
ni Mungu, nafsi ya mwana ni Mungu, na nafsi ya Roho mtakatifu ni Mungu, lakini
hakuna miungu watatu.
Nafsi ya Baba siyo nafsi ya mwana wala nafsi ya Baba siyo nafsi ya Roho mtakatifu, wala nafsi ya mwana siyo ya Roho mtakatifu lakini nafsi zote ni MUNGU mmoja.
AJABU KUU KUHUSU UTATU MTAKATIFU.
Wote wanashirikiana
kufanya wanachotaka, Ukiangalia utashangaa namna ambavyo huu utatu
mtakatifu wanavyoshirikiana kwa kila jambo.
Nataka nikuoneshe kazi
zao kwa ufupi ikifuatiliwa na mifano halisi inayotuelezea haya majukumu yao
yalivyo kaa;
1.
Mungu Baba ndiye mbeba
nia au mbeba maono ya jambo tena anayetoa dira na ramani ya kazi wanayotaka
kuifanya, na ndiyo maana anaitwa BABA huko mbeleni nitakuonesha vizuri maana ya
Baba kwamba ni chanzo.
2.
Mungu Mwana ndiye
mtendaji mkuu wa kazi ya Uungu, katika kila jambo wanalolifanya. Ndiyo maana
anaitwa Neno na ndilo lenye sifa ya kuumba, tutaangalia pia vizuri kule mbele.
3.
Mungu Roho mtakatifu ni
mmaliziaji wa kazi ya waliyoianza Baba na Mwana; ndiyo maana anaitwa msaidizi
(Paraclitus) kwa sababu anakuja kama kusaidia kazi iliyoanishwa tayari na
kuimalizia.
Mfano wa kwanza
(2).
UUMBAJI WA MUNGU.
Wakati Mungu anaziumba
mbingu na nchi, maandiko yanasema Roho wa Mungu alikuwa ametulia juu ya uso wa maji,
ndipo Mungu akawa anatamka Neno na ikawa kama alivyotamka.
Kumbuka ukitaka
kumwelewa Mungu wetu japo kwa mbali kwa ufahamu aliyotupa; hebu turudi
kumwangalia mwanadamu kidogo ambaye ndiye kiumbe pekee aliyeumbwa kwa sura na
mfano wa Mungu.
Mwanadamu anazo sehemu kuu tatu ili akamilike; yaani Roho, nafsi na mwili kama vile Mungu wetu alivyo na nafsi tatu Baba, Mwana na Roho mtakatifu.
Sasa kama ujuavyo mwili
huwa unaongozwa kutenda kile nafsi inachokuwaza wakati huo; vivyo hivyo hapa
najuaa ni ngumu kidogo kumwonesha Mungu wakati akiwaza kwenye uumbaji kwamba
kitokee nini hadi unapoona kimeshaumbwa na nafsi ya pili tayari.
kwa hiyo, unaposikia Mungu akasema na iwe nuru ikawa, maana yake nafsi ya pili ambayo ndiyo mtekelezaji mkuu alikuwa akisikiliza nia ya ndani aliyonayo Baba na kuifanya itokee mara.
Nataka nikuoneshe kwamba
nafsi ya pili Yesu ndiye muumbaji (mtekelezaji mkuu)
Wakilosai 1:15-17 “naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana,
mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa,
vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana;
ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa
kwa njia yake, na kwa ajili yake. Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu
vyote hushikana katika yeye”
Unaposikia kwamba Roho
wa Mungu akatulia juu ya vilindi vya maji alikuwa akisubiri utekelezaji wa
uumbaji ili amalizie kazi hiyo.
Mfano wa pili (2).
KAZI YA UKOMBOZI WA MWANADAMU.
Kimsingi nafsi ya Mungu
Baba ndiyo ilitoa wazo la kuwakomboa wanadamu baada ya kuanguka dhambini na
kutengwa mbali na uso wa Mungu.
Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda
ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali
awe na uzima wa milele”
Kimsingi hapa
anayeongelewa ni Mungu Baba japo wote walikubaliana katika hili kama tulivyoona
kwamba wote wanakubaliana kwa jambo moja kwa sababu wao ni umoja.
Sasa angalia, Nafsi ya pili ya Mungu (Yesu) aitwaye Neno ndiye aliyetumwa kuja kufanya kabisa kazi ya ukombozi na kufa msalabani, kumbuka ndiye mtekelezaji mkuu kwa kila kazi wafanyayo.
Yohana 1:1-3 “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno
alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu.
Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote
kilichofanyika”
Tena angalia mstari wa 14 kwenye kitabu hicho hicho;
Yohana 1:14 “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu;
nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba;
amejaa neema na kweli”
Kumbe mtekelezaji wa ukombozi
wa mwanadamu ni naafsi ya pili ya Mungu kama tulivyoona tena kwenye uumbaji
kwamba ndiye mtendaji mkuu (Chief engineer)
Sasa angalia nafasi ya Roho mtakatifua hapa;
Yohana 16:13 “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa
kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake
mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha
habari yake”
Maana yake kumbe yeye
ndiye anayetukamilisha au kwa maneno mengine ndiye anayekamilisha kazi ya
ukombozi wa mwanadamu ambao ni kazi ya Mungu mwenyewe katika nafsi zote tatu.
lakini Roho mtakatifu
kazi yake sasa ni kukamilisha wale waliyoupokea wokovu ili wakamilike sana
mbele za Mungu wawe wasiyo na lawama wala kunyanzi. Na ndiye aliyeachiwa kanisa
kwa sasa kulisimamia hadi unyakuo utakapotokea.
Kumbuka Mwanadamu
ameumbwa katika sehemu tatu, mwili nafsi na roho na zote hizo zinautofauti wake
na mfanano wake lakini zote tatu kwa pamoja zinaitwa mwanadamu. Uwezi
kusema nafsi yako siyo wewe lakini kimsingi nafsi na roho ni vitu viwili
tofauti vyenye utendaji kazi tofauti, hali kadhalika na mwili.
Vivyo hivyo na Mungu
naye anazo nafsi tatu lakini huwezi kusema ni miungu watatu,
Moja kati ya tabia tuliyoiona kuhusu utatu mtakatifu ni kwamba;
Wote wanapatana kwa
jambo moja (wana nia moja)
1Yohana 5:8 “Kwa maana wako watatu washuhudiao
mbinguni, Baba, na Neno, na Roho Mtakatifu, na watatu hawa ni umoja”
Yesu hawezi kufanya
lolote bila kusikia kutoka kwa Baba na wala Roho mtakatifu haneni kwa shauri
lake mwenyewe hadi asikie kutoka kwa Yesu.
Yohana 12:49 Kwa sababu mimi sikunena kwa nafsi yangu tu; bali Baba aliyenipeleka, yeye mwenyewe ameniagiza nitakayonena na nitakayosema.
Yohana 16:13-15 Lakini
yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa
maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena,
na mambo yajayo atawapasha habari yake. Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa
katika yaliyo yangu na kuwapasha habari. Na yote aliyo nayo Baba ni yangu; kwa
hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasheni habari.
1Yohana 5:8 Kwa maana wako watatu washuhudiao mbinguni, Baba, na Neno, na Roho Mtakatifu, na watatu hawa ni umoja. Kila mmoja anamshuhudia mwenzake.
Baba anamshuhudia mwana
Mathayo 3:17 na tazama,
sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa
naye.
Mwana
anamsuhudia Roho mtakatifu.
Yoh 16:13 Lakini yeye
atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa
maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena,
na mambo yajayo atawapasha habari yake.
Roho
anamshuhudia Mwana
Yoh 15:26 Lakini
ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli
atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia.
Kuna mengine kadri siku zinavyoenda kama nikipata kibali kuhusu utatu mtakatifu nitayaeleza lakini nataka kwanza tupige hatua kidogo leo.
Mungu wetu ambaye ni
mmjoa na wa pekee wa kweli aliye na nafsi tatu (Baba, Mwana na Roho mtakatifu)
anazo tabia nne za kipekee zinazomtofautisha na miungu mingine yote ambayo
ulishawahi kuisikia na ambayo hukuwahi kuisikia lakini ipo. Nataka tuziangalie
kwa ufupi hapa;
TABIA KUU NNE ZA KIPEKEE
ALIZONAZO MUNGU WETU MUUMBA WA MBINGU NA NCHI TOFAUTI NA MIUNGU WENGINE.
1. ANAPATIKANA MAHALI POPOTE MUDA WOWOTE.
Ni Mungu wetu pekee
ndiye anayeitwa OMNIPRESENCE likiwa ni maneno mawili ya kilatini yakimaanisha
anayepatikana mahali popote muda wowote.
Yeye kwa sababu ni Mungu
aliyeziumba mbingu na nchi hakuna chochote kinachoweza kujificha na uso wake
tena popote ulipouumbaji wake naye anapatikana hapo.
Hakuna mungu mwingine
aliyena sifa hizo hata Lusifa (shetani) akiwa sehemu moja hawezi akapatikana
tena sehemu nyingine lakini anachofanya anatengeneza mtandao wake na wakati
mwingine wanapomuita wanafikiri ni yeye kumbe ameweka jini lenye sura yake.
Lakini Mungu wetu yupo kila mahali na tena yupo na kila mtu zaidi hata ya pumzi aliyonayo mtu.
Zaburi 139:7-12 Niende wapi nijiepushe na roho yako?
Niende wapi niukimbie uso wako? Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; Ningefanya
kuzimu kitanda changu, Wewe uko. Ningezitwaa mbawa za asubuhi, Na kukaa pande
za mwisho za bahari; Huko nako mkono wako utaniongoza, Na mkono wako wa kuume
utanishika. Kama nikisema, Hakika giza litanifunika, Na nuru inizungukayo
ingekuwa usiku; Giza nalo halikufichi kitu, Bali usiku huangaza kama mchana;
Giza na mwanga kwako ni sawasawa.
2. NDIYE MUNGU PEKEE MWENYE NGUVU ZOTE.
Jina rasmi kwa kilatini
anaitwa OMNIPOTENT likiwa ni muunganilo wa maneno mawili OWN na POTENT likiwa
na maana ya MWENYE NGUVU ZOTE.
Ni Mungu wetu pekee
ndiye anayeitwa mwenyenzi kwa sababu ni yeye pekee Mungu aliye na nguvu zote na
ambaye nguvu zake hazina mipaka wala kikomo kwake hakuna kushindwa wala
hajawahi kushindwa hata siku moja.
YEREMIA 32:27 Tazama,
mimi ni Bwana, Mungu wa wote wenye mwili; je! Kuna neno gumu lo lote
nisiloliweza?
3 NDIYE MUNGU PEKEE ANAYEJUA YOTE.
Jina lingine
linalotumika ni OMNISCIENCE likiwa na maana ya ajuaye yote.
Mungu wetu muunba wa
mbingu na nchi ndiye Mungu pekee anayejua yote na ufahamu wake hauna kikomo na
wala haushindwi kitu. Hakuna utakachomficha asijue na hakuna kitu kipya
kinachoweza kuvumbuliwa mahali popote asikijue. Hii nayo ni sifa pekee
aliyonayo Mungu wetu. Miungu mingine yote ina ukomo kwenye kujua wanayoyajua.
ZABURI 139:1-6 ” Ee Bwana, umenichunguza na kunijua. Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu; Umelifahamu wazo langu tokea mbali. Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu, Umeelewa na njia zangu zote. Maana hamna neno ulimini mwangu Usilolijua kabisa, Bwana. Umenizingira nyuma na mbele, Ukaniwekea mkono wako. Maarifa hayo ni ya ajabu, yanishinda mimi, Hayadirikiki, siwezi kuyafikia”
4. NDIYE MUNGU PEKEE MWENYE HEKIMA ZOTE.
Hekima ya Mungu wetu
ndiyo hekima ya pekee inayoshinda hekima zote za wanadamu na za miungu mingine.
Hata inafikia mahali biblia inashindwa kuielezea hii hekima ya Mungu jinsi
ilivyo kuu, ikasema;
1Wakor 1:25 Kwa sababu
upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu
zaidi ya wanadamu.
Zaburi 104:24 Ee Bwana,
jinsi yalivyo mengi matendo yako! Kwa hekima umevifanya vyote pia. Dunia imejaa
mali zako.
Furaha
nzuri sana maishani ni kuishi maisha matakatifu yenye kumpendeza Mungu, na njia
rahisi ya kuweza kuishi maisha matakatifu ni kumpatia Yesu maisha yako, yaani
kuokoka. Unapo okoka Yesu anakuwa anayatazama maisha yako kwa ushindi ulio
mkuu, huku akikutakasa kwa ajili ya uzima wa milele.
Kama bado hauja okoka sali sala hii fupi kwa imani, na utakuwa umekoka na kumpokea Roho Mtakatifu huku ukitembea kwa kuishi maisha matakatifu;-
Sema
"Eeh Bwana Yesu, ninakuja mbele yeko, mimi ni mwenye dhambi, nimekutenda
dhambi kupitia matendo yangu, kusema kwangu, kuwaza kwangu na kwa dhambi
za kujua na za kutokujua, Eeh Bwana Yesu ninaomba unisamehe, nisafishe kwa Damu
yako ya thamani, nifute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uniandike jina
langu kwenye kitabua cha Uzima wa milele, Eeh Bwana Yesu nakuja mbele zako
kuanzia siku ya leo nifinyange moyo wangu, nafsi yangu na roho yangu kama
upendavyo wewe, maisha yangu yote nakukabidhi wewe uyaongoze kwa Roho wako
Mtakatifu, naomba na kuamini kupitia Jina la Yesu kristo aliye Bwana na mwokozi
wa maisha yangu. Amina.
Mpendwa
kama umesali sala hii fupi kwa kumaanisha tayari umeupokea wokovu, unatakiwa
utafute kanisa lililo karibu yako lenye kumuabudu Mungu wa kweli na uungane nao
kwa ajili ya kukua kiroho.
Kama
umeguswa chochote kupitia makala hii , naomba uandika ujumbe wako hapo chini na
nitakapo soma nitafurahia sana.
Na kama utahitaji maombi na ushauri wowote wa kiroho, wasiliana nami kupitia namba na emeil yangu kwa njia ya sms. mwishoni nitatoa namba na email, lakini kama umeokoka kupitia makala hii waweza kunitumia ujumbe kwa njia ya simu , kwa watsapp, au kwa kawaida , au kupitia email yangu nitakayo itoa hapo chini.
Somo hili
limeandaliwa na Noel Pallangyo, na kuandikwa na
mwandishi Daniel J Mbugu wa makala ya AMKA
UKUE KIRIHO.
Karibu
katika sehemu ya Tatu ambayo itawekwa kupitia blogu hii. Mungu akubariki sana.
Wako
mpendwa katika Kristo,
Daniel Mbugu.
Kwa
mwendelezo wa mafundisho zaidi ya neno la Mungu tembelea AMKA
UKUE KIRIHO. www.amkaukuekiroho1.blogspot. Na
kwa ushauri kuhusiana na maisha ya wokovu tuma ujumbe katika email
yangu. www.mbugudaniel@gmail.com. Au wasiliana nami
kwa kutuma ujumbe kwa njia ya sms au whatsApp kwa 0758505174/ 0655505173.
Comments
Post a Comment